Thursday, June 10, 2010

HOTUBA YA BAJETI YA SERIKALI 2010-2011

HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA NA UCHUMI, MHE. MUSTAFA HAIDI MKULO (MB.), AKIWASILISHA KATIKA BUNGE MAPENDEKEZO YA SERIKALI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2010/2011, TAREHE 10 JUNI, 2010

UTANGULIZI

1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kujadili na kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2010/2011. Pamoja na hotuba hii, vipo vitabu vinne vinavyoelezea kwa kina takwimu mbalimbali za bajeti. Kitabu cha Kwanza kinahusu makisio ya mapato. Kitabu cha Pili na cha Tatu ni vya makisio ya matumizi ya kawaida kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kitabu cha Nne kinaelezea makadirio ya matumizi ya maendeleo kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Mikoa pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2010 ambao ni sehemu ya bajeti hii.

2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote ningependa kuchukua nafasi hii kueleza kuwa, Bajeti ya mwaka wa fedha 2009/2010 unaomalizika mwezi huu, inakamilisha kipindi cha miaka mitano cha Serikali ya Awamu ya Nne iliyoingia madarakani Desemba 2005. Katika kipindi hiki, Bajeti imetumika kama chombo muhimu katika kutekeleza Sera na Malengo ya Uchumi na Maendeleo ya Jamii kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala cha CCM. Kwa hiyo, bajeti ya mwaka wa fedha 2010/11 inalenga kuendelea na utekelezaji wa sera na malengo ya kiuchumi na kijamii. Katika kipindi hiki, yamekuwepo mafanikio ya kuridhisha katika kutoa huduma bora kwa wananchi na kuimarisha miundombinu ili kuwezesha uchumi kukua na kupunguza umaskini.

3. Mheshimiwa Spika, naomba pia nichukue fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa wale wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine kufanikisha matayarisho ya Bajeti hii. Maandalizi ya bajeti ya Serikali yanahusisha wadau na vyombo mbalimbali. Kipekee ninaishukuru Kamati ya Fedha na Uchumi chini ya uenyekiti wa Dkt. Abdallah Omari Kigoda, Mbunge wa Handeni, pamoja na kamati nyingine za kisekta kwa ushauri mzuri waliotoa wakati wakichambua mapendekezo ya bajeti hii. Naomba niishukuru kwa namna ya pekee Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutayarisha kwa wakati Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2010 na nyaraka mbalimbali za kisheria ambazo ni sehemu ya bajeti hii.

4. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Wizara ya Fedha na Uchumi, nawashukuru Naibu Mawaziri, Mhe. Jeremia H. Sumari (Mb) na Mhe. Omari Y. Mzee (Mb). Namshukuru Katibu Mkuu Ndugu Ramadhani M. Khijjah na Naibu Makatibu Wakuu, Ndugu John M. Haule, Ndugu Laston T. Msongole na Dkt Servacius B. Likwelile, pamoja na Katibu Mtendaji Tume ya Mipango; Dkt. Philip. I. Mpango. Aidha, napenda kuwashukuru Wakuu wa Idara na wafanyakazi wote wa Wizara ya Fedha na Uchumi. Vile vile, namshukuru Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kwa kuchapisha hotuba hii kwa wakati. Mwisho, nawashukuru wataalamu na wale wote waliotoa mapendekezo kuhusu sera, mikakati na masuala mbalimbali ya kodi ambayo yamezingatiwa katika kuandaa Bajeti hii.

5. Mheshimiwa Spika, huu ni mkutano wa mwisho wa Bajeti kwa Bunge hili baada ya miaka mitano ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Nne. Wengi wetu tutarudi kwa wananchi kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi yetu, kuomba ridhaa yao ya kurudi tena katika ukumbi huu. Nina matumaini makubwa kuwa, wananchi hawatasahau kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Awamu hii.

6. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Mkakati wa Taifa wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA); Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs); na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005. Napenda kulipongeza Bunge lako Tukufu chini ya uongozi wako, kwa mchango mkubwa ambao umeiwezesha Serikali kupata mafanikio makubwa katika kipindi hiki.

Mafanikio ya utekelezaji wa Sera za Bajeti na changamoto zilizojitokeza katika kipindi cha Awamu ya Nne

7. Mheshimiwa Spika, yafuatayo ni baadhi ya mafanikio ya Serikali katika kipindi cha kwanza cha Awamu ya nne:

(i) Mapato ya ndani ya Serikali yameongezeka kwa asilimia 121 kutoka shilingi 2,124.8 bilioni mwaka 2005/06 hadi shilingi
4,688.3 bilioni ambazo zinatarajiwa kukusanywa kwa mwaka 2009/10. Mapato ya ndani yamefikia zaidi ya wastani wa shilingi 390 bilioni kwa mwezi ikilinganishwa na wastani wa shilingi 177 bilioni mwaka 2005/06, sawa na ongezeko la zaidi ya mara mbili katika kipindi hicho. Aidha, mapato ya ndani kama asilimia ya Pato la Taifa yaliongezeka kutoka asilimia 12.5 mwaka 2005/06 hadi asilimia 16.4 mwaka 2009/10. Hii imesababishwa na jitihada za Serikali katika kuboresha sera za kodi na usimamizi wa ukusanyaji wa mapato;

(ii) Jumla ya misaada na mikopo ya Bajeti (GBS) iliongezeka kutoka shilingi 588.702 bilioni mwaka 2005/2006 hadi shilingi 1,307.707 bilioni zinazotarajiwa kupatikana kwa mwaka 2009/10. Aidha, misaada na mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo iliongezeka kutoka shilingi 1,047.266 bilioni mwaka 2005/06 hadi kufikia shilingi 2,825.431 bilioni ambazo zinatarajiwa kupatikana kwa mwaka 2009/10. Hii imetokana hasa na utekelezaji wa Mkakati wa Pamoja wa kusimamia Misaada (MPAMITA) pamoja na uhusiano mzuri uliopo baina yetu na washirika wa maendeleo;

(iii) Jumla ya matumizi ya serikali yaliongezeka kutoka shilingi 4,131.946 bilioni mwaka 2005/2006 na matarajio ni kwamba hadi Juni 2010 matumizi yote yatakuwa shilingi 9,238.801 bilioni. Katika kipindi hicho matumizi yalizingatia katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, MKUKUTA, Malengo ya Milenia 2015 na katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005;

(iv) Mikopo iliyotolewa na mabenki kwa sekta binafsi kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi iliongezeka kutoka shilingi 1,571.0 bilioni mwezi Desemba 2005 hadi shilingi 4,836.0 bilioni mwezi Oktoba 2009. Sera sahihi za fedha (prudent monetary policy) zimechangia ongezeko hilo;

(v) Deni la Taifa limepungua kutoka Dola za Kimarekani 10.01 bilioni mwaka 2005/06 hadi kufikia Dola za Kimarekani 8.25 bilioni mwaka 2008/09 sawa na upungufu wa asilimia 18. Kwa mujibu wa mwenendo wa viwango vya deni kuwa himilivu, Deni la Taifa linaonesha kuwa linadhibitiwa na linahimilika;

(vi) Miundombinu ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na barabara, nishati na umwagiliaji imejengwa na kukarabatiwa. Sekta ya elimu imeimarishwa ikiwa ni pamoja na kujenga shule za sekondari za Kata, Chuo Kikuu cha Dodoma na kuvipa hadhi baadhi ya vyuo kuwa vyuo vikuu;

(vii) Mfuko wa Uwezeshaji Kiuchumi umeendelea kuwezesha wananchi kiuchumi kwa kutoa Shilingi 10.5 bilioni katika awamu ya kwanza kupitia mabenki ya CRDB na NMB. Fedha hizo ziliongezwa mara tatu na kufikia shilingi 31.5 bilioni. Aidha, hadi Desemba, 2009 jumla ya wajasiriamali 66,559 walikuwa wamefaidika na mikopo iliyotolewa ikiwa na uwiano wa wanaume 42,851 na wanawake 23,708. Kadhalika, katika awamu ya pili, Serikali imetoa Shilingi 10.5 bilioni; kati ya hizo Shilingi 600 milioni zilipelekwa Zanzibar na Shilingi 9.9 bilioni Tanzania Bara; Vile vile Serikali inatambua na kuthamini mchango wa taasisi zisizo za kiserikali katika kuwawezesha wananchi kama vile FINCA, Presidential Trust Fund (PTF), PRIDE, VICOBA, na kadhalika;

(viii) Mfuko wa uwezeshaji wa wajasiriamali wadogo (Small Enterpreneurs Loan Facility-SELF) umeendelea kutoa mikopo katika kipindi cha Awamu ya Nne. Mwaka 2005 ilitoa mikopo ya shilingi 5.6 bilioni. Hadi kufikia Machi 2010, jumla ya mikopo iliyotolewa ilikuwa shilingi 25.1 bilioni sawa na ongezeko la asilimia 348. Vile vile, taasisi za fedha zilizofaidika na mikopo ya SELF ziliongezeka kutoka 175 mwaka 2005 hadi 247 Machi 2010 sawa na ongezeko la taasisi 72. Idadi ya wanufaika iliongezeka toka 20,526 mwaka 2005 hadi 69,795 mwaka 2010. Kati ya hao wanawake ni asilimia 58;

(ix) Mfuko wa uwezeshaji wananchi kiuchumi ulianzishwa mwaka 2007 kwa mtaji wa shilingi 400 milioni. Mfuko huo umeendelea kutoa mikopo kwa wajasiriamali, ambapo hadi Desemba 2009, mikopo yenye thamani ya shilingi 4.2 bilioni ilitolewa kwa wajasiriamali 4,437 wakiwemo wanawake 1,341 na wanaume 3,096; na
(x) Mfuko wa Udhamini wa mikopo kwa ajili ya mauzo ya bidhaa nje ya nchi (ECGS) na Mfuko wa Udhamini wa wafanyabiashara wadogo na wa kati (SME’s-CGS) imeongeza mitaji kutoka shilingi 500 milioni Septemba mwaka 2005 hadi shilingi 5.751 bilioni mwezi Machi mwaka 2010. Hii imeongeza wigo wa ukopeshaji kwa wafanyabiashara kupitia mabenki husika.

8. Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio niliyoainisha, bado kuna changamoto mbalimbali za kibajeti kama ifuatavyo:

(i) Mapato ya ndani hayawiani na mahitaji ya kugharamia shughuli mbalimbali za Serikali, hususan miradi ya miundombinu ya reli, barabara, bandari, viwanja vya ndege na umwagiliaji; huduma za jamii (elimu, afya na maji); na kilimo;

(ii) Sehemu kubwa ya shughuli zinazohusiana na uchumi wetu kutoingizwa katika sekta rasmi na hivyo kuendelea kuwa na mchango mdogo katika mapato ya ndani;

(iii) Kasi ndogo ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na uelewa mdogo wa Sheria ya Manunuzi ya Umma 2004, kuchelewa kupatikana kwa fedha za maendeleo; na

(iv) Utumiaji wa mfumo wa kutayarisha na kutoa taarifa za hesabu (IFMS) haujasambaa kikamilifu kufikia Halmashauri zote nchini.

9. Mheshimiwa Spika, katika hotuba yangu ya Hali ya Uchumi niliyowasilisha leo asubuhi, nilieleza mwenendo wa uchumi wa nchi tokea mwaka 2005/06 mwanzo wa Awamu ya nne hadi mwaka 2009 na malengo ya uchumi katika kipindi cha muda wa kati (2010/11 – 2012/13). Napenda sasa kuchukua fursa hii kutoa maelezo kuhusu mapitio ya Bajeti ya mwaka 2009/10 katika kipindi cha miezi tisa ya kwanza ya mwaka huu; Mwelekeo wa Bajeti hadi Juni 2010; na Misingi na Shabaha ya Bajeti kwa mwaka 2010/11.
MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA SERA ZA BAJETI YA MWAKA 2009/10
10. Mheshimiwa Spika, Sera za Bajeti kwa 2009/10 zilihusisha sera za mapato ya ndani; matumizi; misaada; na mikopo. Sera za Mapato zilihusisha hatua za kupanua wigo wa mapato; kuimarisha usimamizi na udhibiti wa makusanyo kutoka vyanzo mbalimbali; kuchukua hatua za kupunguza misamaha ya kodi na kuweka vivutio kwa wawekezaji wa ndani na nje.

11. Mheshimiwa Spika, sera za matumizi zililenga kutoa upendeleo wa mgao wa matumizi kwenye sekta za kipaumbele ikiwa ni pamoja na Elimu, Miundombinu na Kilimo. Aidha, Sera za matumizi pia zilihusisha kuimarisha mfumo wa usimamizi wa fedha na ufuatiliaji wa matumizi pamoja na tathmini ya mpango na bajeti ili kuhakikisha rasilimali fedha inatumika kwa ufanisi. Hatua za kibajeti zilichukuliwa kukabiliana na athari zinazotokana na msukosuko wa kiuchumi duniani; kutenga fedha za kugharamia miradi maalum katika maeneo yenye mazingira yasiyovutia watumishi kufanya kazi; kuboresha utoaji wa huduma; na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika programu muhimu za kijamii kama vile afya, elimu, maji.

12. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa misaada na mikopo, Serikali ilidhamiria kutafuta misaada na mikopo yenye masharti nafuu na yenye manufaa ili kuweza kuongeza uwezo wa Serikali kugharamia miradi mikubwa ya miundombinu ikiwa ni pamoja na kushirikiana na sekta binafsi.

13. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia Sera hizo, Serikali ilipanga kukusanya mapato ya jumla ya shilingi 9,513.685 bilioni kutokana na mapato ya ndani, mapato kutoka Serikali za Mitaa, misaada na mikopo ya nje, mikopo ya ndani na mapato ya ubinafsishaji. Aidha, Serikali ilikadiria kutumia jumla ya shilingi 9,513.685 bilioni sawa na mapato yote. Hata hivyo, kufuatia Bajeti ya nyongeza iliyopitishwa na Bunge mwezi Februari 2010, Mapato na Matumizi yaliongezeka kwa kiasi cha shilingi 19.0 bilioni na hivyo kufikia shilingi 9,532.685 bilioni kutokana na mapato mapya.

MAPATO YA NDANI

14. Mheshimiwa Spika, matarajio ya Serikali katika kipindi cha mwaka wa fedha 2009/10 yalikuwa ni kukusanya mapato ya ndani yasiyopungua shilingi 5,096.016 bilioni sawa na asilimia 16.4 ya Pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 15.9 mwaka 2008/09. Ili kuhakikisha kuwa jukumu la kukusanya mapato hayo linatekelezwa kwa ufanisi kama ilivyopangwa, hatua mbalimbali zilichukuliwa ikiwa ni pamoja na:

(i) Kuendelea kupanua wigo wa kodi, kupunguza misamaha ya kodi na kuendelea kuimarisha uchumi tulivu pamoja na kuweka mazingira bora ya biashara ili kuwezesha sekta binafsi kukua;

(ii) Kusimamia kwa karibu mageuzi yanayoendelea ndani ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) chini ya Mpango wake wa Tatu wa Maboresho wa Miaka Mitano (Third Corporate Plan) ambao malengo yake ni pamoja na: kuziba mianya ya ukwepaji kodi; kudhibiti uvujaji wa mapato ya Serikali; kuendelea kutoa elimu ya biashara; na kuimarisha namna ya ukokotoaji kodi kwa wafanyabiashara;

(iii) Kuendelea kurekebisha mfumo wa kodi na kuimarisha Idara ya Walipakodi Wakubwa kwa kuboresha mifumo ya utendaji;

(iv) Kuendelea kuboresha usimamizi na utendaji katika Idara ya Forodha kwa kuongeza uwajibikaji, matumizi ya teknolojia, na kupunguza kero kwa walipa kodi;

(v) Kuendelea kuimarisha usimamizi na udhibiti katika kupeleka mizigo kwenye bandari za nchi kavu (Inland Container Depot - ICD), ikiwemo matumizi ya teknolojia ya kisasa;

(vi) Kuimarisha udhibiti wa bidhaa za mafuta ya petroli, ikiwemo kuhakikisha kuwa, mita za kupitishia bidhaa hizo (flow metres) zinafanya kazi kwa ufanisi wakati wote;

(vii) Kuhakikisha kuwa mafuta yanayopitishwa hapa nchini kwenda nchi jirani (transit goods) hayauzwi katika soko la ndani;

(viii) Kushirikiana na Mamlaka husika ili kudhibiti uchanganyaji wa dizeli na mafuta ya taa kwa lengo la kudhibiti uvujaji wa mapato na kuhakikisha ubora na usalama wa vyombo vinavyotumia dizeli;

(ix) Kuanzisha na kuendesha ghala la forodha kwa ajili ya bidhaa za mafuta (TIPER Fuel Bonded Warehouse). Hatua hii itawezesha kuwa na hifadhi ya mafuta, kudhibiti mapato ya Serikali pamoja na kuongeza ufanisi wa soko la bidhaa za mafuta kwa kupunguza gharama za uagizaji na uendeshaji na hivyo kuweza kushusha bei kwa watumiaji;

(x) Kuboresha ukaguzi wa kodi (field and desk audits) na usimamizi wa ukusanyaji wa malimbikizo ya kodi;

(xi) Kuboresha usimamizi wa mapato ya kodi ya majengo na mapato ya kodi yatokanayo na ukodishaji au upangishaji wa majengo hayo; na

(xii) Kukamilisha tathmini ya utaratibu na utambuzi wa vyanzo vya mapato yasiyo ya kodi kutoka Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea kwa lengo la kubaini upungufu uliopo na kufanya marekebisho ili kuongeza ufanisi na udhibiti wa makusanyo ya mapato hayo.

15. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2009/10, Serikali ilifanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani SURA 148. Marekebisho hayo yalijumuisha kupunguza kiwango kilichokuwa kikitozwa awali cha asilimia 20 ya mauzo hadi asilimia 18 ili kujenga mazingira ya kuongeza kiwango cha ulipaji kodi kwa hiari; kuanza kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye muda wa maongezi kwenye simu kwa kutumia bei halisi inayooneshwa kwenye vocha badala ya bei nafuu anayotozwa muuzaji wa jumla; na kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye huduma za upangishaji na ukodishaji wa nyumba na majengo. Aidha, katika kipindi hicho, Serikali ilitoa msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye matanki maalum ya kuhifadhi maziwa na vipipa vya alumini vinavyotumika kukusanya maziwa kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya vyombo hivyo ili kuongeza ubora wa maziwa na kipato kwa wafugaji. Vile vile, Serikali ilianza kutoa msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye huduma za upakiaji na upakuaji mizigo kwenye meli za mizigo zinazotoka nje ya nchi; pamoja na kutoa msamaha wa kodi hiyo kwenye huduma za kilimo za kutayarisha mashamba, kulima, kupanda na kuvuna ili kupunguza gharama za uzalishaji.

16. Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka 2009/10, Serikali pia ilifanya marekebisho kwenye Sheria ya Ushuru wa Bidhaa SURA 147, kwa kutoza ushuru wa bidhaa katika huduma za simu za mkononi pale vocha ama muda wa maongezi unapouzwa badala ya kusubiri hadi muda wa maongezi utumike.

17. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia matakwa ya Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mawaziri wa Fedha wa Nchi wanachama waliridhia kufanya marekebisho mbalimbali katika Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004 kama ilivyoainishwa kwenye Hotuba yangu ya mwaka 2009/10.

18. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2009 hadi Machi 2010, Serikali ilikusanya mapato ya ndani kiasi cha shilingi 3,490.263 bilioni, sawa na asilimia 91.3 ya lengo la kukusanya shilingi 3,821.397 bilioni. Mwenendo huu unaonesha upungufu wa shilingi 331.133 bilioni ikilinganishwa na lengo. Upungufu ulijitokeza kwenye ushuru wa bidhaa kutokana na kupungua kwa uzalishaji wa bidhaa zinazotozwa kodi hii hasa sigara, bia na vinywaji baridi. Aidha, upungufu katika mapato yasiyo ya kodi ulijitokeza kwenye ada na tozo mbalimbali.

19. Mheshimiwa Spika, mapato kutokana na Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa mauzo ya ndani yalikuwa shilingi 564.798 bilioni, ikiwa ni asilimia 90 ya makadirio. Mapato kutokana na kodi hiyo kwa uagizaji kutoka nje yalifikia shilingi 568.984 bilioni ikilinganishwa na makadirio ya kukusanya shilingi 556.643 bilioni, ikiwa ni asilimia 2 juu ya lengo. Kwa uagizaji kutoka nje, makusanyo halisi ya Ushuru wa Forodha yalikuwa shilingi 282.309 bilioni, sawa na asilimia 90 ya malengo ya kukusanya shilingi 314.251 bilioni. Aidha, mapato kutokana na ushuru wa bidhaa zinazozalishwa nchini yalifikia shilingi 230.846 bilioni, sawa na asilimia 83 ya makadirio ya kukusanya shilingi 278.617 bilioni, wakati shilingi 393.555 bilioni zilikusanywa kutokana na ushuru wa bidhaa zilizoagizwa nje ikilinganishwa na shilingi 448.660 bilioni zilizokadiriwa, sawa na upungufu wa asilimia 12. Makusanyo halisi yanayotokana na vyanzo vya kodi ya mapato yalikuwa shilingi 1,039.887 bilioni, ikiwa ni asilimia 94 ya lengo la kukusanya shilingi 1,108.908 bilioni.

20. Mheshimiwa Spika, makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi yanayokusanywa na Wizara, Idara na Mikoa yalifikia shilingi 160.243 bilioni, sawa na asilimia 80 ya makadirio ya kukusanya shilingi 199.653 bilioni. Upungufu huu unatokana na sababu zilizoelezwa hapo awali. Kwa upande mwingine, kufikia Machi 2010 kiasi cha shilingi 9.659 bilioni zilipatikana kutokana na uuzaji wa baadhi ya hisa za Serikali NMB ambapo lengo lililowekwa kwa mwaka wa fedha 2009/10 ni shilingi 15.0 bilioni. Taratibu zinaendelea ili kuuza bakaa ya hisa hizo kwenye soko la Hisa.

MIKOPO NA MISAADA

21. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2009/10, Serikali ilipanga kukopa shilingi 506.193 bilioni, sawa na asilimia 1.6 ya Pato la Taifa kutoka vyanzo vya ndani ikiwa ni moja ya hatua za kukabiliana na msukosuko wa uchumi duniani. Hadi Machi 2010, kiasi cha shilingi 155.3 bilioni kilikopwa kwa ajili hiyo. Aidha, dhamana za Serikali zenye thamani ya shilingi 424.393 bilioni ziliuzwa katika soko ili kulipia zilizoiva (roll-over) na kusaidia kudhibiti ujazi wa fedha.

22. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2009 – Machi, 2010, jumla ya misaada na mikopo ya bajeti (GBS) iliyopokelewa ilikuwa shilingi 998.676 bilioni sawa na asilimia 84 ya shilingi 1,193.91 bilioni zilizokadiriwa kwenye bajeti. Misaada na mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo (ikijumuisha Mfuko wa Basket) ilifikia shilingi 1,380.883 bilioni, sawa na asilimia 93 ya makadirio katika kipindi hicho.
MATUMIZI

23. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuwianisha matumizi yake na sera za utekelezaji wa MKUKUTA ikiwa ni nguzo muhimu ya kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025. Aidha, bajeti ya mwaka 2009/10 ilielekeza rasilimali zaidi katika elimu, miundombinu, kilimo na afya. Katika kipindi cha Julai 2009 - Machi 2010, matumizi halisi yalikuwa shilingi 6,143.918 bilioni sawa na asilimia 91 ya makadirio ya shilingi 6,718.713 bilioni. Kati ya fedha hizo, shilingi 4,189.721 bilioni ni matumizi ya kawaida na shilingi 1,954.197 bilioni ni matumizi ya maendeleo. Matumizi haya yamegharamiwa na mapato ya ndani, misaada ya nje, mikopo ya ndani na nje.

24. Mheshimiwa Spika, malipo ya mishahara ya watumishi wa Serikali kwa kipindi cha Julai 2009 – Machi 2010 yalikuwa shilingi 1,276.706 bilioni sawa na asilimia 97 ya makadirio ya shilingi 1,320.908 bilioni. Malipo ya riba kwa madeni ya ndani yalifikia shilingi 145.914 bilioni, sawa na asilimia 62 ya lengo la kulipa shilingi 236.638 bilioni na kiasi cha shilingi 27.681 bilioni kilitumika kulipia riba kwa madeni ya nje, sawa na asilimia 73 ya makadirio. Kwa upande wa matumizi ya madeni mengine (CFS Others), jumla ya shilingi 276.569 bilioni zilitumika, ikiwa ni asilimia 81 ya makadirio.

25. Mheshimiwa Spika, matumizi mengineyo katika Wizara, Idara, Taasisi za Serikali, Mikoa na Halmashauri yalifikia shilingi 2,462.851 bilioni sawa na asilimia 97 ikilinganishwa na makadirio kwa kipindi hicho. Mwenendo wa matumizi umekwenda sambamba na upatikanaji wa mapato katika kipindi hicho. Aidha, matumizi ya maendeleo yalifikia jumla ya shilingi 1,954.197 bilioni zikijumuisha fedha za ndani shilingi 625.383 bilioni na shilingi 1,328.814 bilioni fedha za nje, ikiwa ni asilimia 75 na asilimia 93 ya makadirio kwa mtiririko huo.

MASUALA YANAYOHUSU SERIKALI ZA MITAA

26. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2009/10, Serikali Kuu imeendelea kujenga mazingira wezeshi katika Serikali za Mitaa ikiwa ni pamoja na kuzipatia fedha, watumishi, vitendea kazi na ushauri wa kitaalamu kulingana na maeneo yaliyoainishwa kwenye Bajeti. Hadi kufikia Machi, 2010, Serikali za Mitaa zilikuwa zimepokea jumla ya shilingi 1,348.370 bilioni sawa na asilimia 65.9 ya lengo la shilingi 2,044.567 bilioni zilizoidhinishwa na Bunge. Kwa upande wa watumishi, Serikali imeweza kuajiri jumla ya watumishi 394 na kati ya hawa, wahasibu ni 307 na wakaguzi wa ndani 87 ambao wameongeza uwezo wa Halmashauri katika kutekeleza bajeti ya Serikali. Aidha, wakuu wa idara za Halmashauri wapatao 800 walipatiwa mafunzo ya kina juu ya uandaaji, utekelezaji, ufuatiliaji na utoaji wa taarifa za bajeti ili kuongeza uwezo wa kusimamia bajeti katika maeneo yao ya utawala.

27. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mapato ya ndani, Serikali za Mitaa zimeendelea kukusanya mapato kutoka katika vyanzo mbalimbali kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa SURA 290. Katika mwaka wa fedha 2009/10, mapato kutoka Halmashauri yalikadiriwa kuwa shilingi 138.052 bilioni. Hadi kufikia mwezi Machi, 2010, mapato halisi yaliyokusanywa kwenye Halmashauri yalifikia jumla ya shilingi 86.263 bilioni sawa na asilimia 62.5 ya lengo.

28. Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikipeleka fedha nyingi kwenye Halmashauri nchini kupitia idadi kubwa ya Akaunti zilizofunguliwa kwa ajili ya matumizi mbalimbali. Hali hii imesababisha kuwepo kwa akaunti nyingi bila ulazima, kuchanganya fedha katika akaunti zisizostahili, kuongeza mzigo wa kazi za wataalamu katika kufunga hesabu za kila akaunti, na kuongeza gharama za uendeshaji wa akaunti nyingi zisizotumika. Ili kuimarisha usimamizi wa fedha Serikali itaendelea kupunguza Akaunti katika ngazi za Halmashauri kwa lengo la kubakiza akaunti chache.

29. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, baadhi ya Halmashauri zimekuwa na matumizi ya fedha yasiyoridhisha hali inayosababisha kupata hati zenye mashaka au hati chafu. Aidha, fedha nyingi zinazotumwa kwenye Halmashauri, hususan fedha za Maendeleo, zimekuwa zikirundikana kwenye Akaunti bila kutumika kwa wakati na hivyo kuwakosesha wananchi huduma bora katika muda uliokusudiwa. Hatua zitachukuliwa kurekebisha hali hiyo.

30. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutumia teknolojia ya kisasa katika mfumo wa bajeti na uhasibu ujulikanao kama “Integrated Financial Management System – IFMS”. Katika Mfumo huo, jumla ya Halmashauri 87 zimeunganishwa kwenye mtandao wa bajeti ya matumizi (Epicor System) na hatua zinaendelea kuunganisha Halmashauri zilizosalia.

31. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2009/10, Serikali imeanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo unaotekelezwa kwa kuzingatia Sheria namba 6 ya mwaka 2009. Serikali imekamilisha kutoa fedha za Mfuko huo ambazo zitaongeza chachu ya kuchangia miradi mbalimbali ya wananchi.

32. Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kuwa fedha zote zinazopelekwa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa zinatekeleza shughuli zilizokusudiwa, Serikali imeendelea kujenga uwezo wa Idara za Mipango, Uhasibu, pamoja na Ukaguzi wa Ndani. Idara hizi kwa ujumla ndizo husimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma katika Halmashauri na kuhakikisha bajeti inaleta manufaa kwa walengwa kulingana na makusudio ya Serikali.

USIMAMIZI WA FEDHA ZA UMMA

33. Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kwa mwaka 2008/2009 imeonesha kuimarika kwa udhibiti na usimamizi wa Fedha za umma katika Wizara na Idara za Serikali Kuu na kupungua kwa hoja za ukaguzi wa fedha za umma. Taarifa imeonesha kuongezeka kwa Hati Safi za Ukaguzi zilizotolewa kwa Wizara na Idara za Serikali Kuu kutoka asilimia 70 kwa hesabu za mwaka 2007/2008 na kufikia asilimia 86 mwaka 2008/2009. Napenda kupongeza Wizara na Idara hizo zilizopata hati safi katika mwaka huo. Pamoja na kuimarika kwa usimamizi wa fedha za umma, Serikali inatambua kuwa bado upo udhaifu wa usimamizi wa fedha za umma katika Serikali za Mitaa. Kutoimarika kwa usimamizi wa matumizi katika Serikali za Mitaa kumejionesha pia katika taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).

34. Mheshimiwa Spika, kadhalika, taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2008/2009 inaonesha udhaifu katika usimamizi wa fedha za umma katika maeneo yafuatayo: kutofuatwa kwa usahihi kwa uandaaji wa hesabu katika viwango vya kimataifa (IPSAS), kutozingatia sheria na kanuni za ununuzi, mifumo dhaifu ya usimamizi na udhibiti wa mali za Serikali na ukusanyaji wa mapato, udhaifu katika ulipaji wa mishahara, kutotekelezwa kwa wakati mapendekezo yaliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali yaliyotolewa kwenye taarifa zake za miaka ya nyuma. Hatua zinachukuliwa kurekebisha udhaifu huo.

MKAKATI WA KUKUZA UCHUMI NA KUPUNGUZA UMASKINI (MKUKUTA)

35. Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha maandalizi ya MKUKUTA awamu ya pili utakaoanza kutekelezwa mwaka wa fedha wa 2010/11. Maandalizi ya MKUKUTA awamu ya pili ni matokeo ya tafiti mbalimbali na mijadala ya wadau mbalimbali wakiwemo Waheshimiwa Wabunge, Wizara, Idara zinazojitegemea na mikoa, Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Mashirika ya Dini, Wahisani, vyama vya wafanyakazi na sekta binafsi. MKUKUTA II utaendelea kujengwa katika misingi ya matokeo tarajiwa katika nguzo kuu tatu (Kukuza uchumi na kupunguza umaskini wa kipato; kuboresha hali ya maisha na ustawi wa jamii; na utawala bora na uwajibikaji). Msisitizo ukiwa katika kukuza na kusimamia uchumi, kuboresha utoaji huduma za jamii, na kuboresha uratibu wa utekelezaji.
36. Mheshimiwa Spika, kwa miaka mitano ijayo, serikali itatenga fedha kwa ajili ya kugharamia MKUKUTA II hasa vipaumbele vichache katika kukuza uchumi wenye kugusa walio wengi, na kuboresha huduma za jamii. Sekta binafsi pia inatarajiwa kuunga mkono juhudi za Serikali kupitia miradi mbalimbali ikiwemo utaratibu wa PPP. Vipaumbele viko katika misingi mikuu minne: (i) kuendeleza na kuhakikisha matumizi bora ya njia kuu za uzalishaji ikiwemo rasilimali watu, ardhi na mtaji; (ii) kuboresha na kuimarisha taasisi za uchumi; (iii) kujenga na kuimarisha miundo mbinu ya uchumi hasa umeme, maji, barabara, reli, bandari na viwanja vya ndege; na (iv) kuimarisha usimamizi wa uchumi ili kujenga uwezo wa Serikali katika kuwezesha sekta binafsi na sekta nyingine kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na ustawi wa jamii.

MWELEKEO WA BAJETI YA 2009/2010 HADI JUNI, 2010

37. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia maelezo niliyoyatoa kuhusu mwenendo wa bajeti katika kipindi cha miezi tisa hadi Machi 2010, matarajio ni kwamba, hadi Juni 2010, mapato ya ndani yatafikia shilingi 4,688.335 bilioni (trilioni 4.7) ikiwa ni chini ya lengo la bajeti kwa asilimia 8 au shilingi 407.681 bilioni. Baadhi ya wahisani wametoa misaada na mikopo zaidi ya kibajeti (GBS) kuisaidia Serikali kukabiliana na athari za msukosuko wa kiuchumi. Kufuatia hilo, hadi kufikia Juni 2010, misaada na mikopo inakadiriwa kufikia shilingi 1,307.707 bilioni ikilinganishwa na bajeti ya shilingi 1,193.91 bilioni. Ongezeko hili litasaidia kupunguza pengo lililojitokeza kwenye mapato ya ndani. Kwa upande wa misaada na mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo, matarajio ni kwamba fedha zitapatikana kama zilivyopangwa kwenye bajeti. Serikali itaendelea kukopa kutoka soko la ndani kama ilivyopangwa kwenye bajeti ya 2009/10 ili kugharamia matumizi, pamoja na kulipia dhamana za Serikali zinazoiva (roll-over). Kwa upande wa matumizi, Serikali itarekebisha matumizi yake ili kuwianisha na mapato yanayotarajiwa.

MISINGI NA SHABAHA ZA BAJETI KWA MWAKA 2010/11

38. Mheshimiwa Spika, mfumo wa bajeti wa mwaka 2010/11 unazingatia Dira ya Maendeleo ya Taifa, Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA), Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs), Mkakati wa Taifa wa Kudhibiti Madeni, Vipaumbele vya uwekezaji wa umma kama vilivyoainishwa katika Mwongozo wa Mpango na Bajeti mwaka 2010/11-2012/13, na Mkakati wa Pamoja wa Misaada Tanzania (MPAMITA). Misingi na shabaha ya bajeti ya Serikali kwa kipindi cha 2010/11 itakuwa kama ifuatavyo:
(i) Kuendelea kuboresha mfumo wa makusanyo ya mapato ya ndani ikiwa ni pamoja na kupanua wigo wa mapato kwa kuhusisha vyanzo vipya;

(ii) Kuimarisha usimamizi na udhibiti wa makusanyo kutoka vyanzo mbalimbali;

(iii) Kuendelea kuchukua hatua za kudhibiti misamaha ya kodi ili kuongeza mapato;

(iv) Kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa kaulimbiu ya Kilimo Kwanza;

(v) Kuharakisha zoezi la kuanzishwa kwa vitambulisho vya Taifa;

(vi) Kuongeza rasilimali katika utekelezaji wa MKUKUTA II kwa kupeleka rasilimali za kutosha katika maeneo machache yenye kuongeza kasi ya ukuaji uchumi;

(vii) Kutenga fedha za kuiwezesha sekta ya Ardhi kupima na kutenga maeneo kwa matumizi mbalimbali ya ardhi;

(viii) Kulinda na kudumisha mafanikio yaliyopatikana hadi sasa katika sekta za huduma ya jamii (elimu, afya na maji);

(ix) Kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012;

(x) Kuimarisha utawala bora na uwajibikaji;

(xi) Kuboresha maslahi ya watumishi na kupanua ajira;

(xii) Kuhakikisha Uchaguzi Mkuu unatengewa rasilimali za kutosha ili kuwezesha uchaguzi kufanyika kama ulivyopangwa;

(xiii) Kuendelea kuboresha mazingira ya kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje;

(xiv) Kuboresha, kupanua na kukarabati miundombinu ya barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege na miradi ya umeme;

(xv) Kuimarisha sera za fedha ili ziendane na zile za mapato na matumizi zitakazosaidia kupunguza mfumuko wa bei, riba, na kuongeza mikopo kwa sekta binafsi;

(xvi) Kuzipa uwezo Serikali za Mitaa wa kusimamia rasilimali watu na fedha ili ziweze kutekeleza kwa ufanisi maamuzi ya kupeleka madaraka kwa wananchi; na

(xvii) Kutafuta mikopo zaidi yenye masharti nafuu na ya kibiashara kutoka nchi na taasisi mbalimbali duniani ili kuongeza uwezo wa Serikali kugharamia miradi mikubwa ya miundombinu ikiwa ni pamoja na kushirikisha sekta binafsi kwa utaratibu wa ubia (PPP).

SERA ZA MAPATO

39. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2010/11, Sera za mapato zinalenga kukusanya mapato ya ndani yasiyopungua shilingi 6,003.59 bilioni sawa na asilimia 17.3 ya Pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 16.4 kwa mwaka 2009/10. Kati ya kiwango hicho, shilingi 5,652.59 bilioni ni mapato yatokanayo na kodi na shilingi 351.0 bilioni ni mapato yasiyo ya kodi. Mapato kutokana na vyanzo vya Halmashauri yanatarajiwa kuwa shilingi 172.582 bilioni. Aidha, Serikali inategemea kuuza baadhi ya hisa zake katika benki ya NBC kupitia soko la Hisa ambapo kiasi cha shilingi 30 bilioni zitapatikana.

40. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutekeleza sera za kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuweza kugharamia sehemu kubwa ya matumizi ya kawaida. Hatua hizo ni pamoja na:

(i) Kuendelea kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato kwa kuhakikisha kuwa pale inapowezekana malipo yanafanyika kwenye mabenki;

(ii) Kuweka mkakati wa kuboresha huduma za utalii kwa kutathmini hoteli (hotel grading) ili ziwe katika viwango vinavyokubalika kimataifa kwa lengo la kuongeza mapato yatokanayo na ada;

(iii) Kuhimiza utekelezaji wa Sheria ya Fedha inayoelekeza mashirika na taasisi kuchangia katika Mfuko Mkuu wa Serikali;

(iv) Kuendelea kupanua wigo wa kodi kwa kusajili walipakodi wapya na kuimarisha uchumi tulivu pamoja na kuweka mazingira bora ya biashara ili kuwezesha sekta binafsi kukua;

(v) Kuendelea kusimamia kwa karibu mageuzi makubwa yanayoendelea ndani ya Mamlaka ya Mapato Tanzania chini ya Mpango wake wa Tatu wa Maboresho wa Miaka Mitano (Third Corporate Plan) ambayo yamekuwa msingi wa kukua kwa mapato ya ndani mwaka hadi mwaka;

(vi) Kuchukua hatua za kuboresha ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi kutoka Wizara na Idara za Serikali;

(vii) Kupitia upya utaratibu wa kutoa misamaha ya kodi kwa lengo la kuongeza udhibiti; na

(viii) Kuendelea kuhakikisha kwamba watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wanajengewa uwezo kwa kuwapatia utaalam wa kutosha ili kuongeza ufanisi katika ukadiriaji na ukusanyaji wa mapato katika Serikali za Mitaa.

MISAADA NA MIKOPO MIPYA

41. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kupokea misaada na mikopo kutoka kwa Washirika wa Maendeleo. Kwa mwaka 2010/2011 Serikali inatarajia kupokea shilingi 821.645 bilioni ikiwa ni misaada na mikopo ya kibajeti ikilinganishwa na shilingi 1,307.707 bilioni zinazotarajiwa mwaka huu wa fedha. Kupungua kwa misaada na mikopo ya kibajeti kunatokana na baadhi ya wafadhili kutoa fedha zilizokuwa zimepangwa kwa mwaka wa fedha 2010/11, kutolewa katika mwaka wa fedha wa 2009/10 ili kusaidia Serikali kupambana na athari za msukosuko wa kiuchumi duniani kama nilivyoeleza hapo awali. Aidha, kiasi cha shilingi 2,452.908 bilioni zinatarajiwa kupatikana kutokana na misaada na mikopo ya miradi ya maendeleo.

42. Mheshimiwa Spika, napenda kuwatambua washirika wetu wa maendeleo ambao wamekuwa msaada mkubwa katika maendeleo ya nchi. Wahisani hao ni: Uingereza, Denmark, Uholanzi, Ubelgiji, Canada, China, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Italia, Japan, Korea ya Kusini, Kuwait, Norway, Hispania, Sweden, Switzerland, Marekani, India, Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, BADEA, European Union, Global Funds, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Kuwait Fund, Nordic Fund, Opec Fund, Saudi Fund, na Mashirika ya Umoja wa Mataifa. Tunawashukuru sana.

43. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutumia mikopo nafuu na kuanzia mwaka ujao kuanza kutumia mikopo ya kibiashara kwa ajili ya kugharamia bajeti yake ya maendeleo. Hata hivyo, kwa kuzingatia mahitaji makubwa ya kuendeleza miradi ya miundombinu,
Katika mwaka 2010/11, tunatarajia kukopa kutoka soko la ndani na nje kiasi cha shilingi 1,331.2 bilioni ili kukidhi mahitaji makubwa ya kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. Aidha, kiasi cha shilingi 797.6 bilioni zitakopwa kwa ajili ya kulipia dhamana za Serikali zitakazoiva. Serikali itahakikisha kwamba mikopo ya ndani haiathiri utulivu wa hali ya uchumi na kwamba sekta binafsi inapata mikopo kwa riba nafuu ili kuendeleza shughuli zao. Serikali itahakikisha kwamba fedha hizo zinatumika katika miradi ya kipaumbele na yenye tija. Serikali haitakopa mikopo yenye masharti ya kibiashara kwa ajili ya kugharamia matumizi ya kawaida. Uamuzi huu unazingatia kwamba Deni la Taifa linaendelea kuhimilika.

UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI

44. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2010/11, Serikali itaendelea kuratibu utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuhamasisha uanzishwaji wa SACCOS kama njia bora ya kupata mikopo yenye masharti nafuu; kuainisha aina ya mafunzo ya ujasiriamali yanayohitajika kwa lengo la kuendeleza elimu na stadi za ujasiriamali; kutoa mikopo yenye masharti nafuu ili kuwawezesha wajasiriamali wadogo, hususan vijana na wanawake kuanzisha na kuendeleza miradi inayolenga kuongeza kipato, tija na ajira.



MASUALA YANAYOHUSU SERIKALI ZA MITAA

45. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2010/11 Halmashauri zinategemea kukusanya jumla ya shilingi
172.582 bilioni sawa na asilimia 2.9 ya mapato ya ndani yanayokusanywa na Serikali Kuu. Kiasi hiki ni kidogo ikilinganishwa na fursa zilizopo katika mazingira ya Serikali za Mitaa. Katika mwaka ujao wa fedha, Serikali itaendelea kujenga uwezo wa Halmashauri wa kubuni vyanzo vipya vya mapato ikiwa ni pamoja na kuongeza tija katika ukusanyaji wa vyanzo vilivyopo. Serikali itafanya marekebisho ya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa ili kuongeza wigo wa kukusanya mapato zaidi na kuweka ukomo wa mgawanyo wa matumizi ya fedha hizo katika miradi ya maendeleo na matumizi ya kawaida. Aidha, Serikali Kuu itasaidia kutoa mafunzo ya ukadiriaji na ukusanyaji mapato kwa watumishi wanaohusika katika Serikali za Mitaa ili kuwaongezea uwezo zaidi

46. Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kuwa fedha zinazopelekwa kwenye Serikali za Mitaa zinatekeleza shughuli zinazokusudiwa, Serikali itaendelea kuziwezesha na kuziimarisha Idara za Mipango, Uhasibu na Ukaguzi wa Ndani ili kuongeza uwajibikaji, usimamizi na udhibiti wa fedha katika Halmashauri.


SERA ZA MATUMIZI

47. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2010/2011, sera za matumizi ya Serikali zinalenga katika kuboresha usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za umma ili kuongeza ufanisi zaidi pamoja na kutoa kipaumbele kwa maeneo muhimu ya kiuchumi yatakayochochea ukuaji wa haraka wa uchumi na kupunguza umaskini, hususan wa kipato. Aidha, kwa kutambua umuhimu wa Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba 2010, Serikali imetenga fedha za kutosha ili kuhakikisha kuwa, uchaguzi unafanyika kama ulivyopangwa.

Uwianishaji wa Mipango na Bajeti

48. Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kuwepo kwa mipango madhubuti na nidhamu katika usimamizi wa bajeti, hatuna budi kuweka msukumo katika kuimarisha uwianishaji wa mpango wa muda wa kati na bajeti na kuongeza ufanisi katika matumizi ya rasilimali fedha chache za umma. Ili kuongeza kasi ya kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, Serikali kupitia Tume ya Mipango, itaanza kuandaa Mipango ya Muda wa Kati (Medium Term Plans-MTPs) ya miaka mitano mitano.


Maeneo ya Kipaumbele Katika Bajeti ya 2010/11

49. Mheshimiwa Spika, maeneo ya kipaumbele katika bajeti ya mwaka 2010/11 yanazingatia sera za matumizi zilizoelezwa hapo juu. Pamoja na maeneo hayo, Serikali itatoa umuhimu wa kipekee kwa Uchaguzi Mkuu wa Mwezi Oktoba 2010 ili kuhakikisha kuwa unafanyika kama ulivyopangwa. Aidha, Serikali itahakikisha mafanikio yaliyokwishapatikana katika sekta za Jamii (afya, elimu na maji) yanalindwa. Maeneo mengine ya kipaumbele yatakuwa ni pamoja na Kilimo na maendeleo ya Mifugo, Ardhi na maendeleo ya makazi, Viwanda, Maji na Umwagiliaji; Utafiti na maendeleo, Miundombinu ambayo ni barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege na nishati; na utekelezaji wa sera ya kupeleka madaraka Serikali za Mitaa (D by D). Kwa muhtasari maeneo yatakayohusika ni pamoja na:

(i) Kuchukua hatua za kukibadilisha kilimo kuwa cha kisasa zaidi na chenye tija kwa: kusaidia na kuwezesha uzalishaji wa mbegu bora kwa wingi; kuendelea kutoa ruzuku ya pembejeo; kuboresha mfumo wa utoaji taarifa za masoko kwa wakulima; kujenga miundombinu ya masoko; na kuanzisha na kuimarisha shughuli za uongezaji thamani katika mazao ya kilimo;
(ii) Kuimarisha huduma za ugani na kufanya tafiti juu ya uzalishaji wa mbegu bora za mifugo; na kuboresha utoaji wa ruzuku ya madawa ya mifugo na chanjo;

(iii) Kuimarisha na kuendeleza kilimo cha umwagiliaji ili kufikia azma ya Kilimo Kwanza, ikiwemo kujenga mabwawa ya uvunaji maji ya mvua ili kuongeza wigo wa umwagiliaji;

(iv) Kuongeza upatikanaji wa maji mijini na vijijini;

(v) Kuanzisha vituo vya kitaifa vitakavyosaidia upimaji wa ardhi na uchoraji ramani na utekelezaji wa mipango ya kitaifa ya matumizi bora ya ardhi;
(vi) Kuharakisha utekelezaji wa mradi wa Vitambulisho vya Taifa;

(vii) Kulinda na kudumisha mafanikio katika sekta ya huduma za jamii yaliyopatikana hadi sasa;

(viii) Kuelekeza rasilimali zaidi katika kujenga na kukarabati miundombinu ya usafirishaji hasa ujenzi na ukarabati wa barabara na reli; kuimarisha miundombinu ya barabara katika Jiji la Dar es Salaam ili kupunguza msongamano; na kukarabati viwanja vya ndege ili kuifanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha biashara ya usafirishaji wa anga kikanda na kimataifa;

(ix) Kuweka mkazo zaidi katika ufuaji wa nishati ya umeme na kutekeleza miradi mbalimbali kwa kushirikiana na sekta binafsi (PPP) ili kuongeza uwezo wa kuzalisha na kusambaza nishati mijini na vijijini;

(x) Kuendeleza wafanyabiashara wadogo na wale wa kati ili waweze kuongeza ubora na thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini kwa kuwekeza kwenye viwanda vya kusindika mazao, kuwekeza kwenye maghala na maeneo ya viatamizi (incubator sites); Kuendeleza na kuhamasisha matumizi ya teknolojia rahisi na sahihi ya viwanda inayolinda mazingira ikiwa ni pamoja na kuzalisha zana za kilimo; na

(xi) Kuanzishwa kwa Benki ya Kilimo; kuimarisha Benki ya Rasilimali Tanzania na Benki ya Wanawake na kuharakisha utekelezaji wa kutoa huduma ya kukodisha zana za kilimo na ujenzi (financial leasing); na kukamilisha uanzishwaji wa kampuni mahsusi kwa ajili ya kutafuta na kutoa mikopo ya muda mrefu ya nyumba (Tanzania Mortgage Refinance Company- TMRC).

50. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia maeneo ya kipaumbele niliyoyaainisha hapo juu, mchanganuo wa bajeti kwa baadhi ya sekta kwa mwaka 2010/11 ni kama ifuatavyo:

(i) Miundombinu imetengewa shilingi 1,505.1 bilioni ikilinganishwa na shilingi 1,096.6 bilioni mwaka 2009/10 sawa na ongezeko la asilimia 37.3;

(ii) Kilimo kimetengewa shilingi 903.8 bilioni ikilinganishwa na shilingi 666.9 bilioni mwaka 2009/10 sawa na ongezeko la asilimia 35.5;

(iii) Elimu imetengewa shilingi 2,045.3 bilioni ikilinganishwa na shilingi 1,743.9 bilioni mwaka 2009/10 sawa na ongezeko la asilimia 17.2;

(iv) Afya imetengewa shilingi 1,205.9 bilioni ikilinganishwa na shilingi 963.0 bilioni mwaka 2009/10 sawa na ongezeko la asilimia 25.2;

(v) Maji imetengewa shilingi 397.6 bilioni ikilinganishwa na shilingi 347.3 bilioni mwaka 2009/10 sawa na ongezeko la asilimia 14.5;

(vi) Nishati na madini imetengewa shilingi 327.2 bilioni ikilinganishwa na shilingi 285.5 bilioni mwaka 2009/10 sawa na ongezeko la asilimia 14.6; na

(vii) Shilingi 30 bilioni zimetengwa kwa ajili ya utafiti na ufuatiliaji. Maeneo yatakayopata upendeleo katika awamu ya kwanza ni ukarabati wa Miundombinu katika taasisi zinazohusika na tafiti mbalimbali. Katika mwaka huo, Serikali inatarajia kuandaa agenda ya Kitaifa yenye kuonesha maeneo ya kimkakati katika utafiti. Lengo ni kuwa na maeneo machache ambayo yatatusaidia kupata matokeo katika muda mfupi na kwa kutumia gharama zinazohimilika.

Udhibiti wa matumizi ya Serikali

51. Mheshimiwa Spika, ili kuboresha usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za umma, Serikali imedhamiria kutekeleza hatua zifuatazo:

(i) Kudhibiti matumizi ya simu na umeme: Katika eneo hili, Serikali inatumia fedha nyingi kulipa ankara za simu na umeme kwa Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea, Mikoa na Halmashauri nchini. Katika mwaka ujao wa fedha, Serikali kwa kushirikiana na Kampuni za simu na umeme (TTCL, TANESCO) inadhamiria kuanza kutumia mfumo wa malipo kabla ya huduma (kama LUKU) kwa Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea na Mikoa ili kudhibiti ulimbikizaji wa madeni ya huduma hizo. Hatua hii pia inalenga kuyaimarisha mashirika haya kimapato; na

(ii) Kudhibiti Matumizi ya Magari: Katika mwaka wa fedha 2010/2011, Serikali itapunguza idadi ya magari yatakayonunuliwa na itaimarisha Wakala wa Ununuzi na Ugavi Serikalini (GPSA) ili uweze kuratibu ununuzi wa magari ya Serikali, ikiwa ni pamoja na kuainisha aina za magari yatakayonunuliwa kwa lengo la kupunguza gharama za ununuzi, uendeshaji na matengenezo.

52. Mheshimiwa Spika, hatua nyingine zitakazotekelezwa katika mwaka ujao wa fedha ni pamoja na:

(i) Kuhakikisha kwamba, Serikali inalipa posho za nyumba kutokana na uwezo wa bajeti. Posho za nyumba zitatolewa tu kwa wafanyakazi wenye stahili na kwa viwango maalum (specific rate) badala ya asilimia ya mshahara kama ilivyo sasa;

(ii) Fedha zilizopangwa kwa ajili ya posho mbalimbali katika Wizara, Idara za Serikali, Mikoa na Halmashauri zitapunguzwa na kudhibitiwa ili kuepuka matumizi yasiyo ya lazima;

(iii) Kuhakikisha kuwa mfumo wa kutayarisha na kutoa taarifa za hesabu (IFMS) unasambaa katika Serikali za Mitaa zilizobaki. Lengo ni kuhakikisha kuwa fedha zinatumika kama zilivyopangwa;

(iv) Kuendelea kutoa mafunzo kwa Wahasibu na Wakaguzi wa Ndani juu ya uandaaji wa hesabu katika viwango vya kimataifa (IPSAS);

(v) Kuanzia mwaka 2010/11, Halmashauri zinatakiwa kuonesha bakaa katika akaunti ifikapo mwisho wa mwaka wa fedha ili zijumuishwe kwenye bajeti ya mwaka unaofuata kama chanzo cha mapato;

(vi) Katika Mwaka 2010/11, Serikali itatumia utaratibu wa malipo unaosimamiwa na Benki Kuu (Tanzania Interbank Settlement System - TISS) kwa malipo yatakayofanywa na Wizara zote zilizopo Dar es salaam na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ili kuharakisha malipo ya Serikali. Hatua zimechukuliwa kulinda mfumo huo kutokana na athari zinazoweza kutokea;

(vii) Kudhibiti utoaji wa dhamana za Serikali kwa vyombo mbalimbali vya umma ili kuepuka ongezeko lisilohimilika la deni la Taifa; na

(viii) Serikali itakuwa na chombo maalum kitakachosimamia ujenzi na viwango vya majengo ya Serikali ili kuwa na majengo yatakayokidhi viwango (standards) vitakavyowekwa.

53. Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kuendelea kuimarisha usimamizi wa fedha za umma, Serikali imefanya marekebisho kadhaa kwenye Sheria ya Fedha za Umma SURA 348 yatakayowasilishwa kwenye Bunge hili. Marekebisho hayo yataiwezesha Hazina, kupitia Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali, kusimamia matumizi ya Fedha za Umma katika ngazi ya Serikali za Mitaa. Aidha, marekebisho hayo yatawezesha uanzishwaji wa Idara Kuu ya Ukaguzi wa Ndani kitaifa ili kuimarisha utendaji wa Wakaguzi wa Ndani katika Wizara, Idara na Halmashauri. Idara hii itawajibika moja kwa moja kwa Mlipaji Mkuu wa Serikali. Idara ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Hesabu za Serikali, pamoja na kuwa na wataalamu wa ukaguzi wa ndani, itahusisha pia wataalamu wa ukaguzi wa kiufundi (Technical Audit) na Usimamizi wa Mali za Serikali, ili kuiwezesha Serikali kutimiza azma ya kusimamia matumizi ya fedha za umma.

54. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuimarisha ukaguzi wa ndani kwa kutoa mafunzo, kufuatilia kwa karibu matumizi ya Serikali, kufanya uhakiki wa mishahara inayolipwa kwa watumishi wa Serikali na kuitumia kikamilifu Idara ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Hesabu za Serikali inayoundwa kusimamia na kudhibiti fedha za umma. Aidha, uimarishwaji wa Mtandao wa kompyuta wa Mfumo wa Usimamizi wa Fedha (IFMS) katika ngazi zote za Serikali utaendelezwa ili kudhibiti matumizi na kuzuia malimbikizo ya madeni unaotokana na kutotumia Mtandao huu. Pamoja na uimarishaji wa IFMS, Serikali itaanzisha database ya miradi itakayounganishwa na IFMS kwa urahisi wa kufuatilia fedha inayotolewa na kutumika katika miradi hiyo.

Maslahi ya Watumishi

55. Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Nne inatambua umuhimu wa kuwa na maslahi bora ya wafanyakazi katika kuongeza ufanisi na tija. Serikali inachukua hatua za kuboresha maslahi ya wafanyakazi katika mwaka 2010/11. Sanjari na hatua hii, utaratibu wa kuhakiki mishahara utaendelea ili kudhibiti malipo kwa wafanyakazi hewa.

Usimamizi wa Mashirika ya Umma

56. Mheshimiwa Spika, katika miaka ya hivi karibuni, pamejitokeza changamoto nyingi katika kusimamia mashirika na taasisi za umma. Baadhi ya mashirika na taasisi za umma zimeshindwa kujiendesha kwa ufanisi na kuwa mzigo mkubwa kwa Serikali kwa kutegemea ruzuku kutoka Serikali Kuu kinyume na lengo la kuanzisha mashirika na taasisi hizo.

57. Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuboresha usimamizi wa mashirika na taasisi za umma kwa lengo la kuongeza ufanisi, tija, mapato na kupunguza utegemezi wa ruzuku kutoka Serikali Kuu. Katika Mkutano wa 19 wa Bunge uliyofanyika mwezi Aprili, 2010, Serikali iliwasilisha na Bunge kupitisha marekebisho ya Sheria ya Mashirika ya Umma SURA 257 na Sheria iliyoanzisha Ofisi ya Msajili wa Hazina SURA 370. Marekebisho haya yanalenga kuifanya Ofisi ya Msajili wa Hazina kuwa mamlaka inayojitegemea kisheria yenye jukumu la kusimamia utendaji na ufanisi katika mashirika na taasisi za umma. Kufuatia marekebisho haya, muundo wa Ofisi ya Msajili wa Hazina utapitiwa upya ili kuiwezesha ofisi hii kuwa na taaluma za kuwezesha kusimamia kwa karibu zaidi utendaji katika mashirika na taasisi za umma. Serikali itaendelea kufanya tathmini ya mashirika na taasisi zake ili kubaini changamoto zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi kwa lengo la kuimarisha ufanisi katika kusimamia rasilimali za umma.

MABORESHO YA MFUMO WA KODI, ADA, TOZO NA HATUA NYINGINE ZA MAPATO

58. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kupanua wigo wa kodi na kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa mapato ili kuweza kugharamia sehemu kubwa ya bajeti. Aidha, Serikali itaendelea kurejea sheria na taratibu zinazosimamia misamaha ya kodi kwa nia ya kuipunguza na kudhibiti usimamizi wake. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) itaendelea kutekeleza Mpango wake wa Tatu wa Maboresho (Third Corporate Plan) wa Miaka Mitano (2008/09 – 2012/13) ambao ndio umekuwa chachu na msingi wa kukua kwa mapato ya ndani. Vile vile Serikali itaimarisha usimamizi na ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi ili yaweze kutoa mchango mkubwa zaidi katika pato la Taifa.

59. Mheshimiwa Spika, Maboresho hayo yatahusu sheria zifuatazo:-

(a) Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Sura 148;

(b) Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura 332;

(c) Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura 147;

(d) Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, Sura 290;

(e) Sheria ya Magari (Kodi ya Usajili na Uhamisho wa Umiliki wa Magari), Sura 124;

(f) Sheria ya Usalama Barabarani, Sura 168;

(g) Sheria ya Bodi ya Korosho, Sura 203;

(h) Sheria ya Kodi ya Michezo ya Kubahatisha (Gaming Tax), Sura 40;

(i) Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ya mwaka 2004;

(j) Misamaha ya kodi ya Magari kupitia sheria za kodi na matangazo ya Serikali (GNs);

(k) Marekebisho madogo madogo katika baadhi ya Sheria za Kodi;
(l) Marekebisho ya Ada na Tozo Mbalimbali za Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea;

A. Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Sura 148;

60. Mheshimiwa Spika, Kwa kuzingatia azma ya Serikali ya kutoa kipaumbele katika kukuza uzalishaji kwenye sekta za kilimo na mifugo na kuongeza mchango wake kwenye pato la Taifa, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani Sura ya 148, kama ifuatavyo: -

(i) Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye usafirishaji wa mazao ya kilimo kutoka shambani hadi kwenye viwanda vya usindikaji kwa wakulima wenye kilimo cha mkataba wa miwa, mkonge na chai;

(ii) Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye mashine na vifaa vya kukusanya, kusafirisha na kusindika maziwa ili kuhamasisha uwekezaji katika sekta ndogo ya maziwa na kuboresha kipato kwa wananchi. Mashine na Vifaa vitakavyohusika na msamaha huu ni kama ifuatavyo: -
(a) Vifaa maalum vya kubebea maziwa (Milk cans – HS Code. 7310.29.90);
(b) Pampu maalum za kusukuma maziwa (Milk pumps- HS Code no. 8413.81.00);
(c) Bomba maalum la kupitishia maziwa kwenye viwanda vya usindikaji -Milk hoses (HS Code. no 8413.70.20);
(d) Kompresa maalum zinazotumika kwenye vifaa vya kupoza maziwa (Compressors used in refrigerating equipment - HS Code 8414.30.00);
(e) Matanki ya kuhifadhia maziwa (Storage tanks, - HS Code 7309.00.00);
(f) Gari maalum lenye kifaa cha kupoza na kusafirisha maziwa (HS Code 8716.31.90);
(g) Mtambo maalum wa kuchemsha maziwa (Milk pasteurizers - HS Code 8434.20.00);
(h) Kifaa maalum cha kuchekecha maziwa ili kutoa siagi (Butter churns -HS Code 8434.90.00);
(i) Vifaa maalum vya kupoza na kutengeneza ubaridi (HS Code 8415.81.00);
(j) Kifaa maalum cha kukandamiza mabonge ya maziwa na kukamua maji ili kuzalisha jibini – (Chees pressers, HS Code 8434.20.00).

(iii) Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye mashudu kwa ajili ya chakula cha mifugo. Hatua hii inalenga katika kuhamasisha ufugaji bora na kuwawezesha wakulima wa mbegu za mafuta kupata bei yenye tija kwa mauzo ya bidhaa hiyo;

(iv) Kuvipa unafuu maalum wa Kodi ya Ongezeko la Thamani vifaa vinavyouzwa kwa Wataalamu wa mifugo waliosajiliwa kwa kufanya marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ili unafuu huu utolewe katika Jedwali la Tatu (Special Relief Supplies) badala ya Jedwali la Pili (Exempt Supplies) la sheria hiyo;

(v) Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye Zana za kilimo kama vile; kivuna nafaka (combine harvester), pick up balers, hay making machinery na mowers vinavyotumika mahsusi kwenye uzalishaji wa kilimo na mifugo;

(vi) Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani katika usafirishaji wa maua kwa ndege kwenda nje ya nchi;

(vii) Kutoa unafuu maalum wa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye mabanda yanayotumika katika kilimo cha maua (green houses);

(viii) Kutoa unafuu maalum wa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye uuzaji wa bidhaa na huduma zitolewazo kwa wakulima waliosajiliwa au mashamba ya vyama vya ushirika kwa ajili ya kujenga miundombinu ya mashamba kama vile mitaro ya umwagiliaji, barabara za mashambani, ujenzi wa maghala au huduma nyinginezo za namna hiyo; na

(ix) Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye huduma za kuzalisha mifugo (breeding services) kwa njia ya kupandisha mifugo na kutumia mashine maalum za kuzalishia/kutotolea vifaranga (incubators);

(x) Kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa kiwango cha asilimia sifuri kwa vyakula vya mifugo vinavyozalishwa hapa nchini.

61. Mheshimiwa Spika, Aidha napenda kufanya marekebisho ya sheria hiyo ili kuhamasisha uwekezaji na uzalishaji katika sekta ya viwanda hapa nchini kama ifuatavyo:

(i) Kutoa unafuu maalum wa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa waendelezaji (developers) wa maeneo ya uwekezaji ya EPZ/SEZ;

(ii) Kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa kiwango cha asilimia sifuri kwenye usindikaji na uzalishaji wa mafuta ya kula kwa wazalishaji wanaotumia mbegu za mafuta zinazozalishwa hapa nchini;

(iii) Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye Vifungashio vya juisi za matunda na bidhaa za maziwa. Hatua hii inalenga katika kupunguza gharama za uzalishaji na kuboresha thamani ya bidhaa zinazozalishwa kwenye viwanda vya juisi na maziwa hapa nchini; na

(iv) Kurejesha utaratibu wa kutambua baadhi ya vifaa kama bidhaa za mtaji (deemed capital goods) kwa baadhi ya Wawekezaji kwa nia ya kuvipa unafuu wa kodi. Hata hivyo, ili kudhibiti matumizi mabaya ya utaratibu huo yanayoweza kuvujisha mapato, Serikali itaunda Kamati maalum (Inter disciplinary committee) itakayosimamiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kufuatilia na kuratibu mchakato wa utoaji wa unafuu pamoja na udhibiti wa matumizi yake. Aidha, itaandaliwa orodha ya bidhaa husika ili zijulikane waziwazi.

Hatua hizi katika Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa pamoja zitapunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi 2.39 bilioni.


B. Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura 332

62. Mheshimiwa Spika, Napendekeza kufanya marekebisho ya sheria ya Kodi ya Mapato, Sura 332 kama ifuatavyo:-
(i) Kurekebisha kifungu cha 11 cha Sheria ya Kodi ya Mapato ili kuweka wigo wa ukomo (ring fencing) wa maeneo ya uchimbaji wa madini kwa nia ya kudhibiti gharama zinazotakiwa kutolewa katika kukokotoa faida itakayotozwa kodi ya mapato kuwa ni zile za eneo husika tu. Hatua hii itahusisha kampuni zote za Madini;

(ii) Kupunguza kiwango cha chini cha Kodi ya Mapato kwa wafanyakazi kutoka asilimia 15 hadi asilimia 14 sambamba na nyongeza ya kima cha chini cha mshahara kitakachotangazwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma. Lengo ni kuwaongezea kipato na kuwapunguzia mzigo wa kodi watumishi wa umma wenye kipato cha chini; na

(iii) Kwa kuwa bado kuna biashara nyingi zinazofanywa na watu wasiokuwa na namba za utambulisho wa mlipa kodi (TIN), napendekeza kodi ya zuio inayozuiwa na Serikali kwa wauzaji wa bidhaa na watoa huduma wasiokuwa na TIN izuiwe pia na wafanyabiashara wote waliosajiliwa ili kuwahamasisha wasiokuwa na namba za utambulisho kwenda kusajiliwa.

Hatua hizi za Kodi ya Mapato zitapunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi 4.468 bilioni.

C. Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura 147

63. Mheshimiwa Spika, Napendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura ya 147 kama ifuatavyo:-

(i) Kupunguza ushuru wa bidhaa kwenye mafuta mazito ya kuendeshea mitambo kutoka shilingi 97 hadi shilingi 80 ili kupunguza gharama za uzalishaji wa bidhaa hapa nchini; Hatua hii imezingatia dhamira ya Serikali ya kukuza viwanda, ajira na mapato ya ndani. Aidha, punguzo hili limezingatia makubaliano ya Serikali na wenye viwanda ya kupunguza Ushuru huo hadi kuufuta kabisa katika kipindi cha miaka mitatu.

(ii) Kurekebisha kwa asilimia 8 viwango maalum vya ushuru wa bidhaa kwenye bidhaa zinazotozwa ushuru huu isipokuwa zile za mafuta ya petroli. Marekebisho haya yanazingatia kiasi cha wastani wa mfumuko wa bei. Viwango vya sasa na vile vinavyopendekezwa ni kama ifuatavyo: -

(a) Vinywaji baridi kutoka shilingi 58 kwa lita hadi shilingi 63 kwa lita;

(b) Bia inayotengenezwa na nafaka ya hapa nchini na ambayo haijaoteshwa, kutoka shilingi 209 kwa lita hadi shilingi 226 kwa lita;

(c) Bia nyingine zote, kutoka shilingi 354 kwa lita hadi shilingi 382 kwa lita;

(d) Mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 25, kutoka shilingi 1,132 kwa lita hadi shilingi 1,223 kwa lita; na

(e) Vinywaji vikali, kutoka shingi 1,678 kwa lita hadi shilingi 1,812 kwa lita.

(iii) Kurekebisha viwango vya Ushuru wa bidhaa kwenye sigara kama ifuatavyo: -

(a) Sigara zisizo na kichungi na zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka shilingi 5,749 hadi shilingi 6,209 kwa sigara elfu moja;

(b) Sigara zenye kichungi na zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka shilingi13,564 hadi shilingi 14,649;

(c) Sigara nyingine zenye sifa tofauti na (a) na (b) kutoka shilingi 24,633 hadi shilingi 26,604 kwa sigara elfu moja;

(d) Tumbaku ambayo iko tayari kutengeneza sigara (cut filler) kutoka shilingi 12,441 hadi shilingi 13,436 kwa kilo; na

(e) Ushuru wa (Cigar) unabaki asilimia 30.

Hatua hizi katika Ushuru wa Bidhaa kwa pamoja zinatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi 20.042 bilioni.





D. Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, Sura 290

64. Mheshimiwa Spika, Napendekeza kufanya marekebisho yafuatayo katika sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, Sura 290 kama ifuatavyo:-

(i) Kusamehe kodi ya majengo kwenye nyumba wanazoishi wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 60 ambao hali zao za kiuchumi haziwawezeshi kulipa kodi hiyo. Hata hivyo, msamaha huu utatolewa kwa wale watakaothibitishwa na uongozi katika Serikali za mitaa kuwa kweli hawana uwezo wa kulipa kodi husika; na

(ii) Kiwango cha kutoza ushuru wa mazao shambani kiwe kati ya asilimia 3 na asilimia 5 ya bei ya kuuza mazao shambani ili kuzipa fursa halmashauri na serikali za mitaa kutoza ushuru huo kulingana na uwezo na raslimali walizonazo.




E. Sheria ya Magari (Kodi ya Usajili na Uhamisho wa Umiliki wa Magari), Sura 124

65. Mheshimiwa Spika, Napendekeza kufanya marekebisho ya Ada ya Usajili na Uhamisho wa Umiliki wa Magari (Magari na Pikipiki) kama ifuatavyo: -
(i) Ada ya kusajili gari kutoka shilingi 120,000 za sasa hadi shilingi 150,000; na

(ii) Ada ya kusajili pikipiki kutoka shilingi 35,000 za sasa hadi shilingi 45,000.

Hatua hizi katika kuongeza viwango vya Ada za Magari na Pikipiki kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi 3.19 bilioni.

F. Sheria ya Usalama Barabarani, Sura 168

66. Mheshimiwa Spika, Napendekeza kufanya marekebisho yafuatayo katika Ada ya mwaka ya leseni za Magari (Annual Motor Vehicle Licence Fee): -

(i) Gari lenye Ujazo wa Injini 0-500.cc kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 30,000 hadi shilingi 50,000;

(ii) Gari lenye Ujazo wa Injini 501-1500.cc kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 50,000 hadi shilingi 100,000;

(iii) Gari lenye Ujazo wa Injini 1501-2500.cc kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 100,000 hadi shilingi 150,000; na

(iv) Gari lenye Ujazo wa Injini zaidi ya 2501.cc kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 150,000 hadi shilingi 200,000.

Hatua hizi katika kuongeza viwango vya Ada ya mwaka ya leseni za Magari kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi 16.981 bilioni.

G. Sheria ya Bodi ya Korosho – Sura 203

67. Mheshimiwa Spika, Napendekeza kuongeza kiwango cha Ushuru wa kusafirisha nje Korosho ghafi kutoka asilimia 10 hadi asilimia 15 au Dola za kimarekani 160 kwa tani moja kutegemea kiwango kipi ni kikubwa. Lengo ni kulinda viwanda, kuongeza ubora na thamani ya korosho na kukuza ajira kwa wananchi.

Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi 2.613 bilioni.

H. Sheria ya kodi ya michezo ya kubahatisha (Gaming Tax), Sura 40

68. Mheshimiwa Spika, Napendekeza kuongeza kiwango cha kodi inayotozwa kwenye mashine za michezo ya kubahatisha kutoka shilingi 16,000 kwenda shilingi 32,000 na kutoza kodi ya kiwango cha asilimia 13 ya mapato kwenye Mashine ya Tombola (Sloating machine).

Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi 0.5 bilioni.

I. Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ya mwaka 2004

69. Mheshimiwa Spika, Mawaziri wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walifanya kikao cha maandalizi ya Bajeti tarehe 12 mwezi Mei 2010, Kampala-Uganda na kujadili mapendekezo ya marekebisho ya Viwango vya Ushuru wa Forodha kwa mwaka 2010/11 yaliyowasilishwa na Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki; Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda. Aidha, Mawaziri wa Fedha walipitia viwango vya Ushuru wa Pamoja wa Forodha (Common External Tariff) kulingana na matakwa ya Itifaki ya Umoja wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inayoelekeza kwamba Nchi Wanachama zipitie viwango hivyo baada ya miaka mitano.

70. Mheshimiwa Spika, Katika mapendekezo yao, Mawaziri wa Fedha wamezingatia kuwepo na soko la pamoja katika Jumuiya na hivyo walikubaliana kuboresha Sekta za Viwanda, Kilimo na Usafirishaji kama vichocheo muhimu katika kukuza uchumi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Katika Sekta ya Viwanda walikubaliana kufanya marekebisho yafuatayo: -

(i) Kuongeza kiwango cha Ushuru wa Forodha kwenye vipitishi joto au umeme vya Aluminiamu iliyowazi na nyaya (bare aluminium conductors and cables) za HS Code No. 7614.10.00 na 7614.90.00 kutoka asilimia 10 kwenda asilimia 25 kwa lengo la kuvilinda viwanda vinavyozalisha bidhaa hizo katika nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki dhidi ya ushindani usio wa haki kutoka nje;

(ii) Kuongeza kiwango cha Ushuru wa Forodha kwa nyaya za umeme (HS Code 7413.00.90) kutoka asilimia 10 hadi asilimia 25 ili kuwianisha na Ushuru wa Forodha unaotozwa kwa shaba nyekundu (Copper wire) ambayo ni bidhaa shindani na inatozwa Ushuru wa Forodha wa asilimia 25;

(iii) Kuondoa Ushuru wa Forodha unaotozwa kwenye malighafi ambazo hutumika katika uzalishaji wa bidhaa zenye msamaha. Hatua hii inalenga katika kuweka mazingira mazuri ya kiushindani kwa kuwa baadhi ya malighafi hizo hutozwa ushuru wa asilimia 10 au asilimia 25. Aidha, Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zitatakiwa kuwasilisha orodha ya malighafi hizo kwenye Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ajili ya utekelezaji. Kwa kuzingatia makubaliano hayo, wenye viwanda hapa nchini wanatakiwa kupeleka orodha ya malighafi husika Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko ili hatimaye iweze kuwasilishwa kwenye Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki;

(iv) Kupunguza kiwango cha Ushuru wa pamoja wa Forodha kutoka asilimia 10 hadi asilimia sifuri (0) kwa malighafi ya viwanda vya kutengeneza rangi (driers) inayotambuliwa chini ya (HS Code 3211.00.00);
(v) Kupunguza kiwango cha Ushuru wa pamoja wa Forodha kutoka asilimia 10 hadi asilimia sifuri (0) kwa malighafi za viwanda vya saruji (Petroleum coke, not calcined) inayotambuliwa chini ya (HS Code 2713.11.00);

(vi) Kupunguza kiwango cha Ushuru wa pamoja wa Forodha kutoka asilimia 10 hadi asilimia sifuri (0) kwenye malighafi zinazotumika kutengeneza kadi zinazotumiwa na makampuni ya simu kuuza muda wa maongezi (Stamping foils) (HS Code 3212.10.00);

(vii) Kupunguza kiwango cha Ushuru wa pamoja wa Forodha kutoka asilimia 10 hadi asilimia sifuri (0) malighafi ya viwanda vya kutengeneza rangi inayotambuliwa chini ya (HS Code 3212.90.10);

(viii) Kusamehe Ushuru wa forodha kwa kutumia utaratibu wa “Duty remission scheme” malighafi za kutengeneza majalada ya vitabu (textile garments coated with gum) (HS Code 5901.10.00);

(ix) Kusamehe Ushuru wa Forodha kwa kutumia utaratibu wa “duty remission scheme” kwa malighafi za viwanda vya kutengeneza viatu (Looped pile fabrics of manmade fibres) HS Code 6001.22.00;

(x) Kupunguza kiwango cha Ushuru wa pamoja wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia sifuri (0) malighafi za viwanda vya vyuma (HS Code 7210.11.00);

(xi) Kupunguza kiwango cha Ushuru wa pamoja wa Forodha kwenye malighafi za viwanda vya vyuma. (HS Code 7212.10.00); na

(xii) Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 10 badala ya asilimia 35 kwenye ngano inayotambulika chini ya (HS Code 1001.90.20) na (HS Code 1001.90.90) kwa muda wa mwaka mmoja kwa vile bado uzalishaji wa bidhaa hiyo katika nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki haujaweza kukidhi mahitaji ya soko la ndani.

71. Mheshimiwa Spika, Kama nilivyoeleza hapo awali, Mawaziri wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamefanya maamuzi yenye kuboresha Sekta ya Usafirishaji ili iweze kuchangia zaidi katika kupunguza gharama za Usafirishaji na kukuza uchumi. Ili kutekeleza azma hiyo, wamekubaliana kufanya yafuatayo: -

(i) Kuendelea na msamaha wa Ushuru wa Forodha kwa magari yenye uwezo wa kubeba tani 5 lakini yasiyozidi tani 20 kama vile Fuso, Isuzu na mengineyo ya aina hiyo (HS Code 8704.22.00) na hivyo kutoza ushuru wa asilimia 10 badala ya asilimia 25 kwa kipindi cha mwaka mmoja;

(ii) Kuendelea na msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye magari yenye uwezo wa kubeba zaidi ya tani 20 (HS Code 8704.23.90) na hivyo kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia sifuri (0) badala ya asilimia 25;

(iii) Kusamehe Ushuru wa Forodha kwa mabasi yatakayoingizwa nchini Tanzania kwenye mradi wa mabasi ya kwenda kasi (Fast Truck Bus Project). Hatua hii inalenga katika kuondoa adha ya usafiri inayosababishwa na msongamano wa magari ambao unaathiri shughuli za maendeleo (uzalishaji na biashara). Aidha, Serikali inaendelea na ukarabati na upanuzi wa barabara na miundo mbinu ili kuwezesha mradi huo kuanza mapema iwezekanavyo;

(iv) Kusamehe Ushuru wa Forodha kwa waunganishaji wa magari (Motor Vehicles Assemblers); na

(v) Kusamehe Ushuru wa Forodha kwa Matrekta ya kukokota matrela yanayotambulika chini ya (HS Code 8701.20.90).

72. Mheshimiwa Spika, Aidha, hatua za kuboresha kilimo na sekta nyinginezo zimehusisha marekebisho ya sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na viwango vya Ushuru wa Forodha kama ifuatavyo: -

(i) Kusamehe Ushuru wa Forodha kwenye taa/balbu zinazotengenezwa kwa kutumia teknolojia ya Emitting Diodes (LED) kwa lengo la kuhamasisha matumizi madogo ya umeme;

(ii) Kusamehe Ushuru wa Forodha kwenye kuku wazazi (parent stock) (HS Code 0105.99.00) kwa lengo la kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya ufugaji wa kuku. Aidha hatua hii inalenga katika kuhamasisha uagizaji kuku wazazi kutoka nje kwa lengo la kukuza uzalishaji wa kuku wa nyama na mayai hapa nchini;

(iii) Kuendelea na utaratibu wa kutotoza Ushuru wa Forodha bidhaa zinazouzwa kwenye Migahawa ya Majeshi ya Ulinzi na Usalama (Armed Forces Canteen) kwa mwaka mmoja;

(iv) Kurekebisha kifungu kinachosamehe Ushuru wa Forodha wa magari kwenye Jedwali la 5 la sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwa wananchi wanaorejea nchini (returning resident) ili kuweka kipindi cha miaka minne (4) kabla mwombaji hajapata msamaha mwingine wa namna hiyo. Hatua hii inalenga katika kudhibiti matumizi mabaya ya msamaha huu;

(v) Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 (HS Code 2523.29.00) kwenye Saruji kwa muda wa mwaka mmoja. Aidha, stadi itafanywa ili kujua viwango vya uzalishaji, mahitaji na bei ya saruji katika soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo itawawezesha Mawaziri wa Fedha kufanya uamuzi sahihi wa kiwango cha Ushuru wa Forodha kwa bidhaa hiyo;

(vi) Kuendelea kutoza kiwango cha Ushuru wa pamoja wa Forodha cha asilimia 35 au Dola za Kimarekani 0.20 (U$ 0.20) kwa kilo kwa nguo za mitumba (HS Code 6309.00.00). Aidha Nchi wanachama zimekubaliana kupiga marufuku uingizaji wa nguo za ndani (under garments);

(vii) Kupunguza kiwango cha Ushuru wa pamoja wa Forodha kwa Majiko yanayotumia gesi kutoka asilimia 25 hadi asimilia 10 (HS Code 7321.11.00); na

(viii) Kusamehe Ushuru wa Forodha kwa glavu (examination gloves) HS Code 4015.19.00 zinazotumika katika hospitali na maabara.

Hatua hizi katika Ushuru wa Forodha na marekebisho ya viwango vya Ushuru wa Pamoja wa Forodha kwa pamoja zitapunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi 4.175 bilioni.

J. Misamaha ya Kodi ya magari kupitia sheria za kodi na matangazo ya Serikali (GNs)

73. Mheshimiwa Spika, Napendekeza kufanya marekebisho kwenye sheria husika za kodi na matangazo ya Serikali yanayotoa msamaha wa magari kwa walengwa mbalimbali ili kuweka ukomo wa umri wa miaka kumi kwa magari hayo. Lengo la hatua hii ni kupunguza wimbi la uagizaji wa magari chakavu na kuhifadhi/kulinda mazingira.

K. Marekebisho madogo madogo katika baadhi ya Sheria za Kodi

74. Mheshimiwa Spika, Napendekeza kufanya marekebisho mengine madogo madogo yasiyo ya kisera katika Sheria mbalimbali za kodi ili ziwe sanjari na azma ya kurahisisha utekelezaji wake.

L. Marekebisho ya Ada na Tozo Mbalimbali za Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea

75. Mheshimiwa Spika, Napendekeza kufanya marekebisho ya viwango vya ada na tozo mbali mbali zinazotozwa na Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea ili kuvihuisha kulingana na hali halisi ya ukuaji wa uchumi.

M. Tarehe ya Kuanza Kutekeleza Hatua Mpya za Kodi

76. Mheshimiwa Spika, Hatua hizi za kodi zinazopendekezwa zitaanza kutekelezwa tarehe 01 Julai, 2010, isipokuwa pale ilipoelezwa vinginevyo.


MFUMO WA BAJETI KWA MWAKA 2010/11

77. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia sera za uchumi jumla pamoja na misingi na sera za bajeti, Serikali inatarajia kukusanya mapato ya ndani ya jumla ya shilingi 6,003.590 bilioni (trilioni 6.0) katika kipindi cha mwaka 2010/11. Kiwango hiki cha mapato ni sawa na asilimia 17.3 ya Pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 16.4 mwaka 2009/10. Mapato kutokana na vyanzo vya Halmashauri yanakadiriwa kuwa shilingi 172.582 bilioni na mapato kutokana na ubinafsishaji shilingi 30.0 bilioni.

78. Mheshimiwa Spika, Serikali imepanga kutumia jumla ya shilingi 11,609.557 bilioni (trilioni 11.6) katika mwaka 2010/11 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na ya maendeleo. Matumizi haya yatagharamiwa na mapato ya ndani, mikopo ya ndani na nje, pamoja na misaada na mikopo kutoka kwa washirika wa maendeleo.

79. Mheshimiwa Spika, Washirika wa Maendeleo wanatarajiwa kuendelea kuisaidia bajeti yetu mwaka 2010/11 kwa kutupatia misaada na mikopo ya jumla ya shilingi 3,274.553 bilioni (trilioni 3.27). Kati ya fedha hizo, shilingi 821.645 bilioni ni misaada na mikopo ya kibajeti na shilingi 2,452.91 bilioni (trilioni 2.4) ni misaada na mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

80. Mheshimiwa Spika, Serikali inakusudia kukopa kiasi cha shilingi 2,128.832 bilioni (trilioni 2.1) kutoka vyanzo vya ndani na nje. Kati ya fedha hizo, shilingi 797.62 bilioni ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva (Roll-over) na shilingi 1,331.2 bilioni (trilioni 1.3) ni mikopo mingine itakayotumika kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.
81. Mheshimiwa Spika, mfumo wa bajeti umezingatia kwa makini matokeo ya hatua za kodi nilizozifafanua hapo awali. Hivyo, jedwali lifuatalo linaonesha muhtasari wa sura ya bajeti kwa mwaka 2010/11.


SURA YA BAJETI MWAKA 2010/11


Mapato
Shilingi Milioni
A.
Mapato ya Ndani

6,003,590

(i) Mapato ya Kodi (TRA)
5,652,590


(ii) Mapato yasiyo ya Kodi
351,000

B.
Mapato ya Halmashauri

172,582
C.
Misaada na Mikopo ya Kibajeti

821,645
D.
Misaada na Mikopo ya Miradi ya Maendeleo na ya Kisekta

2,452,908

(i) Misaada na Mikopo ya Miradi
1,975,120


(ii) Misaada na Mikopo ya Kisekta
477,788

E.
Mikopo ya Ndani na Nje

1,331,212
F.
Mikopo kulipia dhamana na hatifungani za Serikali zilizoiva (Roll-over)

797,620
G.
Mapato kutokana na Ubinafsishaji

30,000

JUMLA YA MAPATO YOTE

11,609,557
Matumizi
H.
Matumizi ya Kawaida

7,790,506

(i) Deni la Taifa
1,756,044

(ii) Wizara
4,155,768

(iii) Mikoa
119,580

(iv) Halmashauri
1,759,114
I.
Matumizi ya Maendeleo

3,819,051

(i) Fedha za Ndani
1,366,143


(ii) Fedha za Nje
2,452,908
JUMLA YA MATUMIZI YOTE

11,609,557

HITIMISHO

82. Mheshimiwa Spika, Bajeti ya 2010/11 ni mwendelezo wa jitihada za Serikali katika kufikia malengo ya MKUKUTA, Malengo ya Maendeleo ya Milenia, na hatimaye Dira ya Maendeleo 2025. Hata hivyo, ili kufikia malengo yetu mapema zaidi, kila mwananchi anapaswa kushiriki kikamilifu kwa kutumia fursa zinazojitokeza kwa kuzalisha mali na kujiongezea kipato.

83. Mheshimiwa Spika, ushiriki katika uzalishaji kwa wananchi mmoja mmoja au katika vikundi ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wetu. Aidha, sekta za kilimo, mifugo na viwanda zikiboreshwa na kutilia mkazo usindikaji wa mazao ya kilimo, zina nafasi kubwa ya kuchangia Pato la Taifa na kukuza ajira. Bajeti hii pia inalenga kuongeza jitihada za Serikali za kuendeleza ardhi, na kuunganisha nchi yetu kwa njia ya miundombinu ya barabara, reli, mawasiliano na nishati.

84. Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema hapo awali, huu ni mkutano wa mwisho wa Bajeti kwa Bunge hili baada ya miaka mitano ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Nne. Wengi wetu tutarudi kwa wananchi kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi yetu, kuomba ridhaa yao ya kurudi tena katika ukumbi huu. Nina matumaini makubwa kuwa, wananchi hawatasahau kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Awamu hii.

85. Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru kwa namna ya pekee, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake mahiri na kwa kunipa heshima ya kuwa Waziri wa Fedha na Uchumi kwa nusu ya pili ya kipindi cha kwanza cha Awamu ya Nne. Aidha, napenda kumshukuru Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Rais kwa uongozi wake na hasa katika kutatua kero za Muungano. Vile vile, namshukuru Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mb), Waziri Mkuu kwa kusimamia vyema shughuli za Serikali Bungeni na kwa ushirikiano na maelekezo mbalimbali yaliyonisaidia kutekeleza kazi zangu kwa ufanisi. Namshukuru Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendesha Bunge letu kwa viwango vya hali ya juu wakati wote. Nawashukuru Mawaziri wenzangu na Waheshimiwa Wabunge wote kwa ushirikiano walionipa wakati wa kutekeleza majukumu yangu kama Waziri wa Fedha na Uchumi. Na mwisho, nachukua fursa hii kuwashukuru wapiga kura wangu wa jimbo la Kilosa walionipa nafasi ya kuwa Mbunge wao kwa kipindi chote cha miaka mitano, ninaamini kwamba sikuwaangusha.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.






Blog Archive