Monday, February 8, 2010

MATOKEO YA KIDATO CHA NNE TANZANIA SHULE ZA SERIKALI HOI

MATOKEO ya mtihani wa kumaliza kidato cha nne kwa mwaka 2009 yametangazwa jana na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) huku yakionyesha shule za serikali zikiendelea kufanya vibaya kwa kushindwa kuwemo kwenye shule 10 bora huku kiwango cha ufaulu kikizidi kupungua.

Aidha, matokeo ya mtihani huo uliofanyika Oktoba mwaka jana yanaonyesha kushuka kwa kiwango cha ufaulu kwa asilimia 11.2 kwani mwaka 2008 kilikuwa asilimia 83.69 wakati mwaka huu kikishuka hadi kufikia asilimia 72.51

Akitangaza matokeo hayo jana jijini Dar es salam kwenye ofisi za baraza hilo, Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dk. Joyce Ndalichako, alisema watahiniwa 351,152 walisajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha nne, kati yao wasichana ni 167,591 sawa na asilimia 47.73 na wavulana 183,561 sawa na asilimia 52.27 wakati mwaka 2008 watahiniwa 241,472 walisajiliwa.

Alibainisha kuwa watahiniwa 42,672 sawa na asilimia 17.85 wamefaulu katika daraja la kwanza hadi la tatu ambapo wasichana ni 13,788 sawa na asilimia 12.47 na wavulana 28,884 sawa na asilimia 22.48.

Alisema, watahiniwa waliopata daraja la nne ni 130,651 sawa na na asilimia 54.66 wakati waliopata sifuri ni 65,708 sawa na asilimi 27.49 idadi inayoonekana kuongezeka tofauti na mwaka jana.

Akizungumzia hilo, Joyce alisema kati ya shule 10 bora hakuna shule ya serikali hata moja na kueleza kwamba shule zinazoongoza ni zile za seminari na nyingine zinazomilikiwa na watu binafsi.

Katibu huyo alizitaja shule 10 bora zenye watahiniwa zaidi ya 35 kuwa ni Shule ya Wasichana Marian na St. Mary’s Junior Seminary, zote za Bagamoyo; St. James Seminary, Uru Seminary, Anwarite Girls, Maua Seminary na St. Mary Goreti, zote za Kilimanjaro; nyingine ni Don Bosco Seminary ya Iringa; St. Francis Girls ya Mbeya; na Feza Boys ya Dar es Salaam.

Aidha, alizitaja shule 10 bora zenye wanafunzi chini ya 35 kuwa ni Feza Girls; Thomas More Machrina na Hellen’s za Dar es Salaam; Mafinga Seminary na Bethelsabs Girls za Iringa; na St. Joseph-Kilocha seminary ya Kilimanjaro.

Nyingine ni Queen of Apostles Ushirombo ya Shinyanga; Dungunyi Seminary ya Singida; Rubya Seminary ya mkoani Kagera; na Sengerema Seminary ya Mwanza.

Alisema nafasi ya kwanza kwa mtahiniwa aliyefanya vizuri imekwenda kwa msichana Imaculate Mosha kutoka Marian Girls wakati mvulana bora ni Gwamaka Njobelo wa Shule ya Sekondari Mzumbe.

Hata hivyo alizitaja shule zilizoshika mkia zenye wanafunzi zaidi ya 35 kuwa ni Sekondari ya Busi na Jangalo za Dodoma; Sekondari ya Misima, Chekelei na Potwe za Tanga; Sekondari ya Milola na Mandawa za Lindi; Sekondari ya Kiwere ya Tabora; Sekondari ya Msata ya Pwani; na Sekondari ya Masanze ya Morogoro.

Sekondari nyingine zilizofanya vibaya zenye wanafunzi chini ya 35 ni Kizara ya Tanga; na Mingumbi, Nahukahuka, Marambo, Ruponda na Mpunyule zote za Lindi. Nyingine ni Songolo ya Dodoma; Dole ya Zanzibar; Ruruma ya Singida; na Viziwi Njombe ya Iringa.

Pamoja na hayo alisema jumla ya watahiniwa 410 wamefutiwa matokeo yao chini ya kifungu namba 52 cha kanuni za mitihani baada ya kubainika kwamba walifanya udanganyifu.

Aliongeza kuwa watahiniwa 184 walibainika kuwa na makaratasi yenye miandiko tofauti au kuwa na miandiko tofauti katika mtihani wa somo; watahiniwa 141 walikamatwa na wasimamizi ndani ya chumba cha mtihani wakiwa makaratasi yanayohisiwa kuwa na majibu ya somo husika.

Alisema kuwa watahiniwa 64 walibainika kuwa na mfanano usio wa kawaida wa majibu jambo ambalo si rahisi kwa wanafunzi wenye uwezo wa kufikiri tofauti.

“Jamani nawaomba wanafunzi wajitahidi kusoma kwani wakikaa kufikiri mtihani utavuja au watapewa majibu kuna hatari kubwa ya kushindwa kufanya vizuri katika mitihani yao au kukamatwa iwapo wataingia na majibu katika vyumba vya mitihani,” alisema Dk. Ndalichako

Aidha, alisema mwanafunzi mmoja wa Shule ya Sekondari ya Kadoto, aliandika matusi mazito katika mtihani wa Biolojia 1 kitendo ambacho ni kosa kwa mujibu wa kifungu 5 (13) cha kanuni za mitihani.

Alisema, matokeo ya watahiniwa 7,242 yamesitishwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kutolipa ada hasa kwa shule za serikali.

Alisema matokeo ya wanafunzi hao yatatolewa pindi mwanafunzi atakapolipa ada ya mtihani na iwapo katika kipindi cha miaka miwili wahusika watakuwa hawajalipa Baraza la Mitihani la Taifa litafuta matokeo yao.

Hata hivyo, alisema baraza hilo limetoa onyo kali kwa vituo mbalimbali vilivyobainika kufanya udanganyifu na kuvifutia usajili vituo viwili ambavyo ni Sinza Iteba na Dar es Salaam Prime kwa kukiuka taratibu za uendeshaji wa mitihani kwa kuwa na wanafunzi wengi kuliko uwezo wake.

http://196.44.162.32/olevel.htm
http://www.necta.go.tz/html_csee209/olevel.htm

Blog Archive