Thursday, October 8, 2009

B.W. Mkapa


Ingawa yeye mwenyewe amejitahidi kuwa kimya tangu alipomaliza muda wake wa Urais kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania,jina lake limeendelea kuongoza vichwa vya habari mara kwa mara.Kwa bahati mbaya,amekuwa akitajwa kwa mambo ambayo hayapendezi au kutarajiwa kwa kiongozi mstaafu wa nchi inayoimba vita vya umasikini kama Tanzania.Tunamzungumzia Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu,Benjamin William Mkapa.

Amekuwa akitajwa na kuhusishwa na matumizi mabaya ya madaraka na kufanya biashara akiwa Ikulu mahali ambapo Baba wa Taifa,Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere(mwezi huu tunakumbuka kifo chake) alionya kwamba pale sio mahali pa kufanya biashara wala kujipatia utajiri.Baadhi ya Mawaziri wa serikali yake(nakumbuka alipoingia aliwaita “askari wa miamvuli”) tayari wameshafikishwa mahakamani wakikabiliwa na tuhuma mbalimbali nzito za matumizi mabaya ya madaraka na ufisadi kitu ambacho kinazua maswali kama vile,kwanini yeye bado na ikiwa ni msafi,alikuwa wapi wakati mawaziri wake wakitumia vibaya madaraka?

Wiki hii,jina lake limetawala tena vyombo vya habari.Kuna wanaosema wakati umefika sasa kwa Rais Mkapa kufikishwa mahakamani ili “akajisafishe” mwenyewe kwa tuhuma mbalimbali ambazo zimekuwa zikimkabili na kuna ambao(hususani viongozi wa serikali inayotawala-CCM) wanaosema kwamba Mkapa alikuwa kiongozi muadilifu na hivyo hana sababu za kufikishwa mahakamani ukizingatia pia kwamba,kama Rais mstaafu,anayo kinga ya kisheria na kikatiba ya kutokufikishwa mahakamani kwa mambo/hujuma ambazo zilitokea wakati akiwa madarakani.Baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani kama Dr.Slaa wanasisitiza sio tu kwamba ni lazima Mkapa afikishwe mahakamani kujibu tuhuma bali pia anatoa ufafanuzi wa kikatiba kwamba kinga inayosemekana anayo Mkapa,haipo kikatiba.

Kwa mujibu wa maelezo ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Utawala Bora,Sophia Simba,sasa kuna shinikizo kubwa kutoka nje ya nchi(bila shaka kutoka kwa nchi wahisani) linalotaka Rais Mkapa ashitakiwe.

Blog Archive