Sadick Mtulya
UBORA wa noti mpya zilizoanza kutumika mwanzoni mwa mwaka huu unatia shaka, baada ya kubainika kuwa baadhi yake zinachuja na kuacha rangi zikilowa maji au jasho.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Jumapili umebaini kuwa noti hizo hasa za Sh5,000 na Sh10,000 zikikandamizwa au kusuguliwa kwenye karatasi nyeupe hata bila kuloweshwa maji au jasho, huacha rangi. Hali hii imesababisha baadhi ya watu kuanza kutilia shaka ubora wake huku wasomi wakitaka serikali kuwa makini kwa
Lawrence Mkina ambaye Mkazi wa jijini Dar es Salaam aliliambia gazeti hili kwa njia ya simu jana kuwa haamini kama noti mpya kama zina ubora unatakiwa. Alisema aliweka kwenye mfuko wa shti lake jeupe noti za sh 5,000, lakini baadaye alipozitoa shati lilikuwa limechafuka kwa rangi ya noti.
Mkina alisema huenda noti hizo zimechachakuliwa na wanjanja mitaani kwani hata ukiisugua katika karatasi nyeupe zitacha rangi kama ‘carbon paper’. Ili kuthibitisha malalamiko hayo, Mwananchi Jumapili ilichukua noti mpya ya sh 5,000 na kuisugua kwenye karatasi ya nyeupe ikaacha rangi ya bluu.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Honest Ngowi alieleza madhara ya noti zisizokuwa na ubora kuwa ni pamoja na kugushiwa kirahisi.
“Ubora wa noti ni kitu muhimu na kama ikikosa ubora inaleta maswali mengi na moja ya athari itakayojitokeza ni kugushiwa kirahisi,’’ alisema Dk Ngowi. Dk Ngowi ambaye ni mwanazuoni aliyebobea katika taaluma ya uchumi, alisema noti ikikosa ubora, huchakaa mapema na kuleta utata katika kukubalika kwenye soko. “Kutokana na kuchakaa mapema, serikali italazimika kuchapisha noti nyingini hali ambayo italigharimu taifa fedha nyingi katika muda mfupi. Pia inawezekana nchi za Jumuiya ya Afrika ya Afrika Mashariki, zikakataa kuzitumia noti hizo,’’ alisema.
Kuhusu sifa na ubora wa noti, Dk Ngowi alisema ni lazima iwe katika kiwango bora ikiwamo kuwa na karatasi ngumu isiyochakaa na kuchanika mapema na kuwa na uzito. Akizungumzia suala hilo, Gavana wa Benki Kuu, Profesa Benno Ndullu alisema BoT inafuatilia matatizo yanayojitokeza katika noti hizo mpya kwa karibu na kuyafanyia kazi.
“Hili linawezekana ingawa wewe ndio mtu wa kwanza kujitokeza kueleza, lakini kama tatizo hili lipo, tutalifanyia kazi,’’ alisema Profesa Ndullu. Akaongeza: “Kwa sasa BoT ina-monitor (inafuatailia) kwa ukaribu usambazaji wa noti mpya pamoja na kuangalia matatizo yanayojitokeza na kuyafanyia kazi haraka iwezekanavyo.’’ Gavana huyo alisema matatizo yote yatakayojitokeza katika noti hizo yatafikishwa kwa mzabuni aliyezichapisha ili kufanyiwa kazi. Kabla ya kuchapishwa noti hizi, Benki Kuu iliahidi kuwa noti mpya zitakuwa imara ambazo hazitaweza kugushiwa kirahisi.
Tatizo la noti hizo mpya limejulikana siku nne baada ya watu watatu kukamatwa Januari 20, mwaka huu, mkoani Ruvuma wakitengeneza noti za bandia kwenye nyumba ya kulala wageni. Kamanda wa Polisi mkoani humo, Michael Kamuhanda, alisema watu hao ambao wote ni wakazi wa eneo la Bombambili, walikamatwa saa tano usiku katika nyumba hiyo iliyopo Mtaa wa Matomondo, eneo la Misufini. Alisema siku ya tukio, polisi wakiwa kwenye doria waliwakamata watuhumiwa hao wakiwa na karatasi zinazodaiwa kutumika kutengenezea noti bandia.